BARAZA LA WAFANYAKAZI NI KAMA BUNGE :JAJI MAGOIGA

Imewekwa: 22 Feb, 2025
BARAZA  LA WAFANYAKAZI NI KAMA BUNGE  :JAJI MAGOIGA

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro Mhe. Stephen Magoiga, amesema baraza la wafanyakazi ni chombo cha kisheria chenye dhamana ya kutimiza wajibu kama bunge la wafanyakazi kwa ngazi ya taasisi kama ilivyo wabunge kwa ngazi ya majimbo maana linawakilisha mawazo ya wengi.

Ameyasema hayo wakati akifungua kikao cha baraza la wafanyakazi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi kilichofanyika leo tarehe 19 Februari, 2025 Mkoani Morogoro.

Amebainisha kuwa jukumu la msingi la Baraza la wafanyakazi ni kushauri menejimenti katika maeneo mbalimbali ya utekelezaji wa majukumu ambayo taasisi ina wajibika kwa umma na kujadili bajeti ya taasisi na utekelezaji wake kwa kila mwaka wa fedha.

Ametoa rai kwa baraza hilo kufanya wajibu wake  kwa ujasiri na umakini ili kulinda haki na wajibu wa wale waliowachagua kwa maslahi mapana ya Taifa la Tanzania.

Aidha ametoa wito kwa wajumbe wote kusoma kwa makini mkataba wa baraza hasa sehemu ya wajibu ili mara zote wanapokutana wajue wanayopaswa kuyafanya.

"Sisi kama watumishi wa Umma tunawahakikishia watanzania usalama kazini na wawekezaji watapata uhakika wa mazingira rafiki ya uwekezaji nchini"amesema.

Aidha,ameihakikishia Tume kuwa Mahakama itaendelea kutoa ushirikiano wote unaohitajika ili kufanikisha Tume inatekeleza wajibu wake katika kutoa haki kwa jamii ya wafanyakazi na waajiri.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Wafanayakazi ambae pia Mkurugenzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Mhe. Usekelege Mpulla, amemshukuru Mhe.Jaji Stephen Magoiga na kumhakikishia kuendelea kutimiza wajibu kwa kufuata taratibu na sheria.