KAMISHNA WA KAZI AHIMIZA ELIMU YA MFUMO WA e-Utatuzi

Imewekwa: 30 Apr, 2026
KAMISHNA WA KAZI AHIMIZA ELIMU YA MFUMO WA e-Utatuzi

Na Mwandishi Wetu, Njombe

Kamishna wa Kazi, Bi. Suzan Mkangwa, ahimiza  Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), kuendelea kutoa elimu kuhusu matumizi ya mfumo wa usajili wa mashauri ya usuluhishi na uamuzi unaojulikana kama e-Utatuzi ili kuongeza uelewa kwa Wadau.

Bi. Mkangwa ametoa wito huo  Aprili 26, 2026 alipotembelea banda la Tume  katika maonyesho ya Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi yanayofanyika mkoani Njombe katika viwanja vya Shule ya Msingi Mji Mwema.

Akiwa katika banda hilo, Bi. Mkangwa alipata maelezo kuhusu namna mfumo wa e-Utatuzi unavyofanya kazi pamoja na mwitikio wake kwa jamii kwa kuwa mfumo huo unarahisisha usimamizi na uendeshaji wa mashauri ya kikazi, mdaawa anaweza kusajili na kufuatilia mwenendo wa shauri lake popote alipo bila kulazimika kufika ofisi za Tume kwa kutumia kifaa chochote chenye intaneti na unaongeza uwazi na uwajibikaji katika utoaji wa haki.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni: “Mazingira Bora ya Kazi Kisaikolojia ni Njia ya Kuimarisha Ustawi wa Wafanyakazi na Kujenga Taasisi Imara.