Historia yetu

Mnamo mwaka 1984 Tanzania ilibadilisha mfumo hodhi wa uchumi kuelekea mfumo unaoongozwa na soko. Mchakato wa maboresho ulijumuisha dhana ya ubinafsishaji na uchumi wa soko huria ambazo kimsingi zilipelekea kufanyika kwa maboresho katika mfumo wa sheria. Kwa msingi huo, sheria za zamani zilirekebishwa na/au kufutwa na sheria mpya zilitungwa na kujumuisha sheria za kazi.

Maboresho ya sheria za kazi yaliyofanyika yalipelekea kuvunjwa kwa Mabaraza ya Usuluhishi, Mahakama ya Kazi (ya zamani) pamoja na kuondolewa majukumu ya Waziri wa Kazi katika kutatua migogoro ya kikazi, na kupelekea kuundwa kwa taasisi mpya. Mwaka 2004, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga sheria mpya za kazi ili kukidhi mahitaji ya mfumo wa kiuchumi na kijamii tulionao sasa hapa nchini. Sheria hizo ni Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, Namba 6 ya mwaka 2004, Sura ya 366 ya sheria za Tanzania [Toleo la Marejeo la mwaka 2019], na Sheria ya Taasisi za Kazi, Namba 7 ya mwaka 2004, Sura ya 300 ya sheria za Tanzania [Toleo la Marejeo la mwaka 2019].

Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) ni mojawapo ya Taasisi sita zilizoundwa na kupewa jukumu la kutatua migogoro ya kikazi.

Tume ilianza kazi tarehe 04 Mei, 2007 na inatoa huduma katika mikoa yote Tanzania Bara

.

.