MFUMO WA USIMAMIZI MIGOGORO YA KIKAZI KIDIJITALI  MBIONI KUKAMILIKA

Imewekwa: 02 May, 2025
MFUMO WA USIMAMIZI MIGOGORO YA KIKAZI KIDIJITALI  MBIONI KUKAMILIKA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema serikali ipo katika hatua za mwisho katika kukamilisha mfumo wa usimamizi wa migogoro ya kazi kidigitali kwa upande wa sekta binafsi(OCMS).

Ameyasema hayo wakati wa maadhimisho ya  sherehe za Siku ya wafanyakazi Duniani yaliyofanyika kitaifa Mkoani Singida katika uwanja  wa Bombardier, Mei Mosi 2025.

"Aidha kwa upande wa migogoro ya wafanyakazi wa sekta binafsi, Serikali ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha mfumo wa usimamizi wa migogoro ya kazi kidijitali ambao utawaondolea wadau adha ya kupoteza muda na gharama katika kufuatilia huduma hiyo ".

Vile vile Mhe. Rais amesema kulikuwa  na manung'uniko ya uchelewaji wa mashauri yanayofika kwenye Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), hivyo ili kuleta  ufanisi serikali imeandaa mfumo wa kieletroniki  unaolenga kuimarisha shughuli za Tume  na utarahisisha usimamizi na uendeshaji mashauri kwa kupunguza muda na gharama na kusaidia kutatua migogoro ya wafanyakazi kwa haraka.

Naye Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Kanda ya Afrika Mashariki Bi. Caroline Mugalla, akiwasilisha salamu za shirika hilo amesema ILO imeendelea kushirikiana na Mahakama ya Kazi, LESCO na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Ili Kuboresha utatuzi wa migogoro ya kikazi na kukuza mahusiano Bora kazini.