e-utatuzi KUONGEZA UFANISI WA UTATUZI WA MIGOGORO

Imewekwa: 22 Jan, 2026
e-utatuzi KUONGEZA UFANISI WA UTATUZI WA MIGOGORO

Na Mwandishi Wetu,

Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Usekelege Mpulla ameeleza kuwa mfumo wa kieletroniki wa Usimamizi wa Mashauri ya Usuluhishi na Uamuzi (e- Utatuzi) ambao umeanza kutumika rasmi leo Januari 21,2026 utasaidia kuongeza ufanisi katika utatuzi wa migogoro ya kazi kutokana na mashauri yote ya migogoro ya kazi kuendeshwa kidijitali.

Akizungumza mkoani Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi wa matumizi rasmi ya mfumo huo Mpulla ameeleza kuwa mfumo huo pia utasaidia kusogeza huduma kwa jamii, kupunguza gharama za uendeshaji wa mashauri na gharama za kusafiri umbali mrefu kwenda kusajili migororo katika maneo mbalimbali nchini.

Aidha, amesema kuwa mfumo umeleta mapinduzi makubwa ya kidijiti katika kutatua migororo ya wafanyakazi huku akieleza kuwa tangu kuanzishwa kwa CMA mwaka 2007 hadi mwaka 2022 mashauri ya migogoro yalikuwa yakiendeshwa kwa nakala ngumu.

Ameongeza kuwa katika kipindi chote cha matumizi ya nakala ngumu kulikuwa na mrundikano wa majalada ya migororo, hivyo kuleta changamoto ya kutokupatikana kwa wakati pindi yanapohitajika huku akieleza kuwa mfumo huo utaondoa changamoto hiyo na kuongeza ufanisi kwa kutatua migogoro yote ya wafanyakazi kwa wakati.