ILO KUSHIRIKIANA NA CMA KUIMARISHA MIFUMO YA KUZUIA NA KUTATUA MIGOGORO YA KAZI
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Kanda ya Afrika Mashariki, Caroline Mugalla, amesema shirika hilo litaendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania katika kuimarisha mifumo ya kuzuia na kutatua migogoro ya kazi, pamoja na kuhakikisha utekelezaji wa viwango vya kazi unafanyika kwa mujibu wa mikataba ya ILO.
Caroline ametoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa mfumo wa kielektroniki wa e-Utatuzi, uliofanyika leo Januari 21, 2026 mkoani Dar es Salaam.
Amesema uzinduzi wa mfumo huo ni sehemu muhimu ya mkakati wa ILO wa kuzuia na kutatua migogoro katika maeneo ya kazi, huku akisisitiza kuwa shirika hilo litaendelea kuwaongezea ujuzi wasuluhishi na waamuzi ili kuhakikisha viwango vya kimataifa vya kazi vinafuatwa.
Pia, Mkurugenzi huyo ameipongeza Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kwa kuanzisha mfumo wa e-Utatuzi, akisema tume hiyo imeonyesha mfano mzuri kwa nchi za Afrika Mashariki katika kumaliza migogoro kwa haraka na kwa haki.
