e-utatuzi KULETA MAPINDUZI KATIKA UTOAJI HAKI KAZI

Imewekwa: 22 Jan, 2026
e-utatuzi KULETA MAPINDUZI KATIKA UTOAJI HAKI KAZI

Na Mwandishi Wetu,

Dar es Salaam.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina, amesema  mfumo wa e-Utatuzi unaleta mapinduzi ya kidijitali kwa kuongeza uwazi, kasi na ufanisi katika utoaji wa haki kazi.

Mhe.Dkt. Mliyambina ameyasema hayo Januari 21, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla ya kuanza rasmi matumizi ya mfumo wa e-Utatuzi.

Aidha amesema kuwa moja ya faida kuu za matumizi ya mfumo wa kieletroniki wa Usimamizi wa Mashauri ya Usuluhishi na Uamuzi (e-Utatuzi) ni kuwezesha usikilizaji wa migogoro hata katika vipindi vya majanga.

Yose ametoa mfano wa kipindi cha janga la UVIKO-19, akieleza kuwa wadau pamoja na watumishi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) walilazimika kubaki majumbani hadi hali ilipotengamaa, hali iliyokwaza kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa haki na utatuzi wa migogoro wakati huo.

Akizungumza leo Januari 21, 2026 katika hafla ya uzinduzi wa matumizi rasmi ya mfumo huo, amesema e-Utatuzi sasa itawezesha mashauri ya migogoro ya wafanyakazi kusikilizwa muda wowote bila kuathiriwa na hali au janga lolote.

Aidha, ametaja faida nyingine kuwa ni kupunguza gharama za uendeshaji wa mashauri pamoja na kuokoa muda wa kufungua mashauri, kutokana na mdau kuweza kufungua shauri mahali alipo na wakati wowote, tofauti na awali ambapo ilimbidi kufika katika ofisi za Tume na kutumia gharama kubwa ikiwemo za usafiri na matumizi mengine.

Faida nyingine alizozitaja ni kuzuia upotevu wa nyaraka za mashauri, kupunguza mrundikano wa majalada katika ofisi za CMA, pamoja na kuimarisha uwazi na uwajibikaji kwa waamuzi na wasuluhishi katika hatua zote za utatuzi wa migogoro.