JAJI ROSE EBRAHIM AFUNGUA  MAFUNZO YA WAAMUZI MOROGORO

Imewekwa: 07 May, 2025
JAJI ROSE EBRAHIM AFUNGUA  MAFUNZO YA WAAMUZI MOROGORO

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro Mhe. Rose Ebrahim,  amefungua mafunzo ya Waamuzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), yaliyoandaliwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) Kwa kushirikina na Tume hiyo,Mei 6,2025 Mkoani Morogoro.

Akifunga mafunzo hayo Jaji Ebrahim, ameipongeza CMA na ILO kwa kuandaa mafunzo hayo , akisisitiza kuwa uamuzi bora wa migogoro ya kazi ni kichocheo kikubwa cha maendeleo ya uchumi na utulivu wa kijamii.

Aidha amesisitiza umuhimu wa kutoa haki kwa wakati, kuepuka urasimu na kuhakikisha weledi katika ushughulikiaji wa mashauri ya kazi.

““Ni matumaini yangu kuwa ujuzi mtakaoupata hapa utaboresha utendaji wenu katika maeneo mbalimbali ya sheria na kuleta ufanisi zaidi katika utawala wa haki za kazi,” alisema Jaji Ebrahim.

Vile vile ameipongeza Tume kwa uanzishwaji wa mfumo wa usajili wa migogoro ya kikazi kidijitali (OCMS), ambao utarahisisha usajili, usimamizi na ufuatiliaji wa kesi za migogoro ya kikazi na kuongeza ufanisi wa utoaji haki.

Kwa upande wa ILO akimuwakilisha Mkurugenzi Mkazi Kanda ya Afrika Mashariki wa Shirika hilo, Afisa Programu Mwandamizi Bw. Edmund Moshy, ameishukuru CMA kwa uongozi thabiti na ushirikiano endelevu.

Pia amesema mafunzo hayo yataongeza maarifa, kuboresha utendaji kazi na kuchangia katika mfumo bora wenye ufanisi na unaoaminika wa utatuzi wa migogoro ya kazi hapa Tanzania.

Naye Mkurugenzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) Mhe. Usekelege Mpulla amesema anathamini ushirikiano wanaopata siku zote  kutoka ILO na kuandaa mafunzo hayo ambayo yataboresha utendaji kazi,  na utatuzi wa migogoro hapa Tanzania utakuwa wa viwango vinavyohitajika si tu kitaifa bali na kimataifa.