SANGU AIPONGEZA CMA KWA MAFANIKIO YA e-Utatuzi

Imewekwa: 30 Apr, 2026
SANGU AIPONGEZA CMA KWA MAFANIKIO YA  e-Utatuzi

Na Mwandishi Wetu, Njombe

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu  Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu, ameipongeza Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kwa maendeleo makubwa ya mfumo wa e-Utatuzi.

Mhe. Sangu alitoa pongezi hizo alipotembelea banda la CMA katika maonyesho ya Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi yaliyofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Mji Mwema Mkoani Njombe Aprili 29.2026.

Akizungumza katika banda hilo Mhe. Sangu alisema mfumo wa e-Utatuzi umepokelewa vizuri na wadau mbalimbali na umeongeza ufanisi katika kushughulikia migogoro ya kikazi.

“Mfumo wa e-Utatuzi umepokelewa vizuri, pongezi kwenu kwa timu nzima ya CMA," alisema Mhe. Sangu.

Aidha aliitaka CMA kuendelea kuongeza juhudi za kuutangaza mfumo huo kwa waajiri na wafanyakazi ili waweze kuuelewa na kuutumia ipasavyo na kusaidia kurahisisha  maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo aliahidi na ametekeleza.

Mfumo wa e-Utatuzi umeongeza ufanisi na uwajibikaji katika utatuzi wa migogoro ya kazi kwa kuwezesha wadaawa kusajili na kufuatilia mashauri yao kwa njia ya mtandao bila kulazimika kufika katika ofisi za Tume na  kurahishisha utatuzi wa Migogoro kwa haraka.