KAMATI YA BUNGE YAPONGEZA MAFANIKIO YA MFUMO wa e-Utatuzi
Na Mwandishi - CMA
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Hawa Mchafu imempongeza Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha kuanzishwa kwa Mfumo e-Utatuzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) ambao umeongeza ufanisi katika usimamizi wa mashauri ya migogoro ya kazi nchini.
Pongezi hizo zimetolewa Machi 18, 2026 wakati wa ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya mfumo huo ambapo imeelezwa kuwa idadi kubwa ya mashauri yaliyosajiliwa tangu mfumo huo uanze imeongezeka mara mbili zaidi ikilinganishwa na hapo awali.
"Tija ya mfumo tumeiona ni mara mbili ya kile kilichokuwa kinafanyika mara ya kwanza, ubora wa Mfumo umekuwa mara mbili yake" amesema Mwenyekiti wa kamati hiyo.
Aidha ameongeza mfumo huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kuchochea ukuaji wa uchumi, kwani wafanyakazi na waajiri hawatalazimika tena kupoteza muda mwingi kwenye foleni au kufuatilia kesi zao kwa kusafiri umbali mrefu, badala yake watasajili na kufauatilia mashauri yao popote walipo na wakati wowote.
Awali akizungumza Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe.Rahma Kisuo amemshukuru Mhe. Rais kwa kutekeleza ahadi aliyoitoa mwaka jana katika Maadhimisho ya ya siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) ya kuanzisha mfumo huo ambao umesaidia kutatua changamoto zilizopelekwa kwake za Wananchi na Waajiri kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za Tume, Kupoteza muda na gharama kufuatilia haki, Mrundikano wa Mashauri na ucheleweshaji haki na huduma za Tume kukosekana katika baadhi ya Wilaya ambazo hamna ofisi.
Amebainisha kuwa serikali ilikuja na mfumo huo kama suluhusu ya changamoto tajwa kwa ajili ya kurahisisha upatikanaji wa haki mahali pa kazi, kusogeza huduma karibu na wafanyakazi na waajiri ambao ni nguzo muhimu katika ukuaji wa uchumi nchini.
Naye Mkurugenzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Bw. Usekelege Mpulla, amesema kuwa Tume ina mkakati wa kuendelea kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo mbalimbali vya habari na majukwaa mengine ili kuongeza uelewa na matumizi ya mfumo huo kwa wafanyakazi na waajiri wengi zaidi.
MWISHO
