CMA MWALIMU USAJILI MIGOGORO YA KIKAZI KIDIGITALI AFRIKA MASHARIKI -MKURUGENZI MKAAZI ILO

Imewekwa: 29 Aug, 2024
CMA MWALIMU USAJILI MIGOGORO YA KIKAZI KIDIGITALI AFRIKA MASHARIKI -MKURUGENZI MKAAZI ILO

Na Mwandishi wetu,

Dar es salaam

 

Mkurugenzi Mkaazi wa shirika la kazi Duniani (ILO), Ukanda wa Afrika Mashariki Bi. Caroline Mugalla, amesema Tume ya Usuluhishi na Uamuzi  -CMA itakua mwalimu katika kufundisha nchi nyingine kwenye matumizi ya Mifumo ya kusajili na kutatua migogoro ya kikazi.

Ameyasema hayo leo Agosti 26, 2024 Jijini Dar es salaam katika hafla ya ufunguzi wa mafunzo ya mfumo wa kusajili migogoro kwa njia ya mtandao (Online Case management System
(OCMS), kwa wadau mbalimbali na vyama vya wafanyakazi.

Bi. Caroline amesema mfumo huo utamwezesha mwananchi kufungua mgogoro popote alipo nchini na kusaidia kupunguza gharama za kutembea umbali mrefu kwa ajili ya kutatuliwa mgogoro wa kikazi.

Aidha amesema Tanzania itakuwa darasa  kwa  nchi zilizo mbioni kuanzisha mifumo kwa ajili ya kushughulika na utatuzi wa migogoro ya kikazi kwani tayari itaweza kutambua changamoto na namna gani ya kukabiliana nazo huku.

Naye Mkurugenzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Mhe. Usekelege Mpulla amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kuipatia CMA Zaidi ya bilioni mbili kwaajili ya kusimika mfumo huo.

Aidha amesema kukamilika kwa mfumo huo kutasaidia kuongeza ufanisi wa utendaji kazi ikiwa ni Pamoja na kusajili na kutatua migogoro kwa wakati jambo ambalo litasaidia kurahisisha utoaji wa huduma kwa wafanyakazi na waajiri nchini.

Vilevile ameongeza kuwa mfumo huo ni kwaajili ya wananchi na unalengo la kuboresha Zaidi huduma na kuzisogeza karibu kwa wananchi ili kuweza kusaidia upatikanaji haki kwa wakati.