CMA YAPATA DARASA KUTOKA CCMA YA AFRIKA KUSINI
Na Mwandishi wetu,
Dodoma.
Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), imefanya kikao na tasisi ya CCMA ya nchini Afrika Kusini kwa lengo la kujifunza na kupata ujuzi Zaidi kutoka kwa taasisi hiyo yenye majukumu sawa na CMA katika utatuzi wa migogoro ya kikazi.
Kikao hicho kilichofanyika leo Agosti 20,2024 katika ofisi za Tume makao makuu,kwa njia ya mtandao kikihusisha menejimenti ya Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Pamoja na Mkurugenzi mkuu wa taasisis ya CCMA na wajumbe wengine kutoka CCMA.
Akizungumza mara baada ya kikao hicho Mkurugenzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA),Mhe. Usekelege Mpulla, amesema kabla ya kuanzishwa ilitumia tasisi hiyo katika kujifunza namna ya uendeshaji na utatuzi wa miogogoro, hivyo kuendelea kuitumia kwa lengo la kupata uzoefu itasaidia pia katika ukuaji wa CMA.
“Wenzetu wameshapiga hatua katika masuala ya utatuzi wa migogoro ya kikazi na hasa katika haya mambo ya mifumo ya kusikiliza migogoro kwa njia ya mtandao hivyo kwa kuendelea kuwa nao na kufanya mazungumzo ,mbalimbali tutaweza kujifunza mengi kutoka kawao”amesema Mpulla.
Aidha, ameongeza kuwa vikao hivyo vitakua vikiendelea mara kwa mara na tayari wamekwisha kukubaliana kukutana ili waweze kubadilishana uzoefu katika utatuzi wa migogoro kutokana na hatua ambayo tayari CCMA imefikia itakayowezesha na CMA kukua Zaidi.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Usuluhishi CMA, Mhe. Rodney Matalis amesema ushirikiano wa Tume na CCMA utainufaisha Tume hasa katika kuboresha huduma zake kwa upande wa usuluhishi na namna wanavyo endesha taasisi jambo ambalo linatarajiwa kuleta faida na kusaidia kuongeza uzoefu kwa CMA.
“Lengo kubwa ni kujifunza kutoka kwao kwani hata ukiangalia katika masuala haya ya mfumo tayari wamekwisha kufika mbali ukilinganisha na sisi na katika muundo wao na namna ya utendaji kazi kama tasisi ili tuweze kupata uzoefu”amesema Matalis.
Kwaupande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Uamuzi CMA, Mhe. Valensi Wambali, amesema kwa kushirikiana na CCMA kutaleta mafanikio kwa CMA kwani CCMA ina wigo mpana katika utatuzi wa migogoro na inatumia njia tatu ambazo ni Upatanishi,Usuluhishi,na Uamuzi jambo ambalo litawafanya wazidi kupata uzoefu kutoka kwa taasisi hiyo.
“Wenzetu wanaifuata migogoro hukohuko iliko hasa ile yenye maslahi mapana na vilevile wana kazia hukumu na wana maamuzi ya aina tatu ambayo ni Uamuzi unaotokana na Usuluhishi,Uamuzi,na amri shurutishi”amesema.
Aidha ameongeza kuwa ushirikiano na CCMA utaisaidia CMA katika kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu utatuzi wa migogoro na namna wanavyotunza data mbalimbali zinazotokana na shughuli wanazofanya, hivyo itaongezea Tume uzoefu kutoka kwa taasisi hiyo ambayo inachukuliwa kama mfano katika utatuzi wa migogoro ya kikazi.