CMA YASAINI MKATABA WA USHIRIKIANO NA TIC

Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), imesaini makubaliano ya ushirikiano na kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), yenye lengo la kusaidia kutatua changamoto zinazowakumba wawekezaji wa nje na ndani ya nchi, leo Mei 2,2024, jijini Dar es salaam katika ofisi za makao makuu ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC.
Akizungumza kabla ya utiaji saini, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bw. Gileadi Teri, amesema hatua hiyo ni maagizo ya Rais samia katika kuhakikisha wanatatua changamoto zinazowakumba wawekezaji nchini bila kujali ni kutoka ndani au nje ya nchi.
Aidha, amesema changamoto za migogoro ya kikazi zinawakabiliki wawekezaji wa ndani na nje kwani hata watanzania walioajiri hukumbana na changamoto za migogoro mahala pa kazi hivyo kwa kushirikiana na Tume ya USuluhishi na Uamuzi itasaidia kuboresha mazingira bora ya wawekezaji.
Mkurugenzi mtendaji TIC ameongeza kuwa, ushirikiano huo utasaidia kuongeza uelewa kwa kuhakikisha elimu inayohusu migogoro ya kikazi inatolewa kwa wawekezaji nchini kwa kushirikiana na CMA, ili kuwawezesha wawekezaji kufanya shughuli zao kwa kuzingatia sheria na kanuni ikiwa ni pamoja na kuwasaidia kuzitambua sheria vyema na kufahamu wajibu wao.
Vilevile, Teri amesema makubaliano haya pia yanalenga kukuza majadiliano ambayo yatafanyika baina ya CMA, TIC pamoja na wawakilishi wa wafanyakazi kuwepo na namna ya kukaa mezani na kufanya majadiliano kabla ya faini kubwa zinazoweza kutolewa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi CMA, Mhe. Usekelege Mpulla, amesema ushirikiano huo ni katika kuunga mkono serikali ya awamu ya sita kwa kuvutia wawekezaji nchini, hivyo kujipanga kutoa huduma bora ili kuungana na Rais Samia Suluhu Hassan, katika kukuza sekta ya uwekezaji Tanzania.
Usekelege ameongeza kuwa ushirikiano huo utasaidia utatuzi wa migogoro ya kikazi kwa haraka na haki, ili wawekezaji waweze kutumia muda mwingi kuzalisha badala ya kufuatilia migogoro ya kikazi kwa muda mrefu, badala yake itawezesha wawekezaji kuendelea na shughuli za kimandeleo kwaajili ya kukuza Uchumi wa nchi.
