ILO YAIPA KONGOLE CMA USAJILI MIGOGORO KIDIGITALI

Imewekwa: 30 Jul, 2024
ILO YAIPA KONGOLE CMA USAJILI MIGOGORO KIDIGITALI

Shirika la kazi duniani ILO, limeipongeza Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kwa kuanzisha mfumo mpya wa kusajili migogoro ya kikazi kwa njia ya mtandao.

Pongezi hizo zimetolewa leo Julai 30,2024, jijini Dar es salaam na Bi. Noreen Toroka, ambaye ni Meneja wa Mradi wa Kigoma Pamoja, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Shirika la kazi Duniani nchini,  wakati akitoa salamu za shirika hilo kwa watumishi wanaoshiriki mafunzo ya mfumo mpya wa kusajili migogoro unaofahamika kama Online Case Management System (OCMS).

Aidha Bi. Noreen amesema CMA kupitia mfumo mpya wa kusajili migogoro ya kikazi ni dhahiri kuwa inaendelea kutendea haki viwango vya kazi kwani inatoa fursa ya upatikanaji haki kwa wafanyakazi kupitia njia ya mtandao jambo ambalo linaleta tija katika upatikanaji wa haki za wafanyakazi nchini.

Ameongeza kuwa mfumo huu utasaidia pia kuondoa uoga kwa baadhi ya wafanyakazi ambao wamekuwa wakishindwa kudai haki zao kutokana na hofu ya kufahamiana na watu au hata kuwa na hisia za kukosa haki zao pale wanapokutana na changamoto mbalimbali mahala pa kazi.

Naye Mkurugenzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Mhe. Usekelege Mpulla, amelishukuru shirika la kazi Duniani kwa kuendelea kuwa wadau muhimu kwa Tume ikiwa ni pamoja na kushirikiana katika maeneo mbalimbali.

Vilevile Mhe. Mpulla amewataka watumishi walioshiriki mafunzo hayo kutumia fursa hiyo ili kuweza kusaidia kuongeza ufanisi na utendaji kazi wa CMA katika kuboresha huduma na utoaji haki kwa wananchi.