KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YAITAKA CMA KUTOA ELIMU MAHALA PA KAZI
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Dkt. Regina Malima, ameielekeza Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kuongeza jitihada katika kutoa elimu kwa waajiri, wafanyakazi, na wadau wengine kuhusu sheria za kazi, haki, na wajibu katika mahusiano ya kazi.
Akizungumza Leo oktoba 13, 2026 jijini Dodoma wakati wa kikao cha kamati hiyo kilichopokea taarifa ya mwenendo wa utatuzi wa migogoro ya kazi kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2024/25 hadi Septemba 2026, Mhe. Malima amesema elimu hiyo itasaidia kuzuia migogoro isiyo ya lazima na kupunguza migogoro katika maeneo ya kazi nchini.
Aidha, ameishauri Tume hiyo kushirikiana kwa karibu na vyama vya wafanyakazi ili kuhakikisha elimu inafika kwa walengwa kwa haraka na kwa ufanisi zaidi.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri, Mhe. Dkt. Eveline Munisi, akijibu hoja zilizowasilishwa na wajumbe wa Kamati hiyo, ameeleza kuwa Serikali imepokea mapendekezo yote yaliyowasilishwa na itayafanyia kazi kwa lengo la kuboresha utendaji kazi na kuimarisha ufanisi katika mfumo wa utatuzi wa migogoro ya kazi nchini. Vilevile, ameishukuru Kamati hiyo kwa ushirikiano na usimamizi wake thabiti.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa CMA, Mhe. Mpulla Nashon, akiwasilisha taarifa ya utendaji, alieleza mwenendo mzuri wa usajili wa mashauri, usuluhishi, utoaji wa maamuzi na utekelezaji wake huku akiipongeza Kamati kwa usimamizi wake mzuri.
Mhe. Mpulla alitaja vipaumbele vya Tume hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027 kuwa ni pamoja na kuboresha zaidi utoaji wa huduma kwa kutumia Mfumo wa e-Utatuzi, ambao umesaidia kurahisisha upatikanaji wa huduma, kupunguza mrundikano wa mashauri na kuongeza ufanisi kwa ujumla
