WATUMISHI WAPYA CMA WAASWA KUZINGATIA MAADILI YA UTUMISHI WA UMMA
Na mwandishi wetu,
Morogoro
Watumishi wapya wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) wametakiwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ili kuhakikisha wanatoa huduma bora, kwa haki na weledi kwa wananchi wanaofika CMA kupata huduma.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Bw. Usekelege Mpulla, wakati akifungua mafunzo elekezi ya awali kwa watumishi wa umma yanayofanyika mkoani Morogoro leo, Oktoba 20, 2026.
Bw. Mpulla amesisitiza kuwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma ni msingi muhimu katika kujenga utendaji bora, uwajibikaji na uaminifu kwa taasisi za umma. Ameeleza kuwa watumishi wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.
Aidha, amewataka watumishi hao kujiepusha na vitendo vinavyokiuka maadili ya utumishi wa umma, akibainisha kuwa vitendo hivyo vinaweza kuharibu taswira ya taasisi, kuchochea vitendo vya rushwa na kusababisha uvunjifu wa sheria na taratibu za utumishi wa umma.
Amesisitiza umuhimu wa watumishi kuwa waadilifu, waaminifu, wenye nidhamu na kuwajibika katika nafasi zao za kazi, huku wakihakikisha wanawatendea wananchi kwa usawa bila upendeleo wowote katika utoaji wa huduma.
Mafunzo hayo elekezi yanalenga kuwajengea watumishi wapya uelewa kuhusu majukumu yao, mifumo ya utendaji kazi serikalini pamoja na misingi ya utumishi wa umma, ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kuzingatia viwango vinavyotakiwa.
Kupitia mafunzo hayo, watumishi wapya wanatarajiwa kupata uelewa mpana kuhusu wajibu wao kwa taasisi na wananchi, hali itakayosaidia kuimarisha uwajibikaji, weledi na utoaji wa huduma bora katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA).
