WAZIRI SANGU AWATAKA MAKAMISHNA WAPYA KUJA NA MIKAKATI YA KUPUNGUZA MIGOGORO YA KAZI

Imewekwa: 26 Nov, 2026
WAZIRI SANGU AWATAKA MAKAMISHNA WAPYA KUJA NA MIKAKATI YA KUPUNGUZA MIGOGORO YA KAZI

 

Na: Mwandishi Wetu – Dar es Salaam

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, amewataka Makamishna wapya wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kuja na mikakati ya kupunguza migogoro ya kazi inayofikishwa katika Tume hiyo, pamoja na kushirikiana nayo kutoa elimu kuhusu utatuzi wa migogoro kwa vyama vya wafanyakazi na waajiri wanaowawakilisha.

Ametoa wito huo leo, Novemba 26, 2026, wakati wa hafla ya uzinduzi wa Bodi ya Makamishna wa Tume na Kamati ya Huduma Muhimu, inayofanyika jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Mikutano wa NSSF.

Aidha, amemtaka Mwenyekiti wa Tume kuhakikisha CMA inaimarisha utoaji wa huduma kwa njia za kidijitali, akitolea mfano wa Mahakama Kuu ya Tanzania, ili kurahisisha upatikanaji wa haki na huduma mbalimbali za Tume.

“Nimejulishwa kwamba ni mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa CMA kupata kiongozi ambaye ni Jaji, na tunajua Mahakama inafanya vizuri sana katika utoaji wa huduma, ikiwemo matumizi ya mifumo ya kidijitali. Hivyo, tunatarajia mafanikio yaliyopatikana Mahakamani tutayashuhudia yakitokea pia CMA,” amesema Waziri Sangu.

Vilevile, amewapongeza Makamishna waliomaliza muda wao kwa mchango wao katika kuimarisha utendaji wa Tume, hususan kuanza kutumika kwa mfumo wa e-Utatuzi ambao hadi sasa umesajili jumla ya migogoro 3,885.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CMA, Mhe. Jaji Mstaafu Wilfred Dyansobera, akizungumza kwa niaba ya Makamishna wa Tume, amemshukuru Waziri Sangu kwa kuwakumbusha wajibu wao na maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku akiahidi ushirikiano katika kuhakikisha Tume inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Awali, Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Bw. Idris Mvura, ameiomba Serikali kuiwezesha Tume kupata bajeti ya kutosha ili kutekeleza majukumu yake bila vikwazo vya kifedha na kibajeti