MHE. SERERA AITAKA CMA KUSOGEZA HUDUMA MIGODINI

Imewekwa: 10 Jul, 2024
MHE. SERERA AITAKA CMA KUSOGEZA HUDUMA MIGODINI

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, Mhe. Suleiman Serera,ameitaka Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA),kusogeza huduma katika maeneo ya migodi ili kuweza kusaidia wafanyakazi na waajiri katika maeneo hayo kupata huduma ikiwepo elimu kuhusu migogoro ya kikazi kwa urahisi.

Wito huo ameutoa alipotembelea banda la CMA, lililopo katika banda jumuishi la ofisi ya Waziri mkuu katika maonesho ya 48 ya sabasaba yanayofanyika jijini Dar es salaam.

Vilevile ameipongeza CMA kwa kuendelea kusuluhisha na kuamua migogoro ya wafanyakazi na waajiri katika maeneo mbalimbali nchini hasa kwa njia ya usuluhishi ambao ni Rafiki katika kuboresha na kukuza uchumi wan chi.

Aidha ameitaka CMA kuendelea kutoa elimu itakayowasaidia wafanyakazi Pamoja na waajiri kwani wengi hukosa elimu na kujikuta katika changamoto za migogoro ya kikazi kutokana na ukosefu wa elimu jambo ambalo limekua hilisababisha baadhi yao kukosa haki zao wanapokumbana na changamoto makazini.

Serera ameongeza kuwa, kwa kuhakikisha elimu inatolewa itasaidia kutatua changamoto za migogoro inayotokana na kutokupewa mikataba na waajiri ambayo imekua ikijitokeza katika maeneo mengi ya migodi ambayo huchangiwa na ukosefu wa elimu katika maeneo hayo.

Tume ya Usuluhishi na Uamuzi inajishughulisha na utatuzi wa migogoro ya kikazi Tanzania bara ambapo inafuata hatua mbili ambazo ni uamuzi na usuluhishi katika utatuzi wa migogoro ili kujenga uhusiano mwema kazini.