MKURUGENZI CMA ASISITIZA MAADILI KWA WATUMISHI WAPYA
Na Mwandishi Wetu,
Morogoro.
Mkurugenzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Mhe. Usekelege Mpulla, amewataka watumishi wapya wa Tume hiyo kuzingatia maadili, uadilifu na uongozi bora katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Mhe. Mpulla amezungumza hayo wakati wa ufunguzi wa Mafunzo Elekezi ya Awali ya Utumishi wa Umma Oktoba 22, 2025, Mkoani Morogoro.
Aidha amesema kuwa watumishi wa CMA ni miongoni mwa kundi maalum la watumishi wa umma wenye wajibu wa kuzingatia maadili, kwani taasisi hiyo ni chombo cha kimkakati kinachosimamia masuala ya haki za waajiri na waajiriwa.
Vile vile amesisitiza kuwa ufanisi na uadilifu katika kazi ni kinga dhidi ya vitendo vya rushwa na ukiukwaji wa sheria, huku akiwasihi watumishi hao kutumia nafasi walizopewa kwa uaminifu na uwajibikaji mkubwa.
Sambamba na hayo ametoa pongezi kwa Kitengo cha Utawala na Rasilimali Watu kwa kuandaa mafunzo hayo, na kuwashukuru wahadhiri pamoja na wawezeshaji kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kwa kuwapatia washiriki uelewa na maarifa kuhusu Utumishi wa Umma kwa ajili ya ustawi wa Taasisi na Taifa kwa ujumla.
