WANANCHI WAPATA ELIMU YA MIGOGORO WIKI YA VIJANA
Wananchi mbalimbali wamejitokeza kutembelea banda la Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) katika Maonyesho ya Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa 2026, yanayofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Ndua, Sumbawanga, mkoani Rukwa leo Oktoba 10, 2026.
Kupitia banda hilo, wananchi wamepata elimu kuhusu majukumu ya CMA, haki na wajibu wa wafanyakazi na waajiri, aina za migogoro ya kikazi inayoweza kuwasilishwa mbele ya Tume, taratibu za usuluhishi na uamuzi, pamoja na matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa e-Utatuzi.
Ushiriki wa CMA katika maadhimisho haya unalenga kutoa uelewa kwa vijana kuhusu Sheria za Ajira na Mahusiano Kazini, kutambua haki na wajibu wao, na kujua taratibu sahihi za utatuzi wa migogoro ya kikazi ili kuchangia kujenga mahusiano bora kazini kwa ukuaji wa uchumi.
CMA inaendelea kusogeza huduma na elimu kwa wananchi, kwa ajili ya kuimarisha uelewa wa utatuzi wa migogoro ya kazi.
Maadhimisho haya yanaongozwa na kaulimbiu
“Mazingira Tofauti, Fursa Sawa kwa Vijana.”
