WAZIRI SANGU AIPONGEZA CMA KWA KUSULUHISHA MIGOGORO YA KAZI 4339

Imewekwa: 15 Dec, 2025
WAZIRI SANGU AIPONGEZA CMA KWA KUSULUHISHA MIGOGORO YA KAZI 4339

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu, ameipongeza Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kwa kufanikisha kusuluhisha migogoro ya kazi 4,339 hadi kufikia Septemba 2025.

Pongezi hizo amezitoa  Desemba 12, 2025 jijini Dodoma wakati wa mwendelezo wa ziara yake ya kutembelea taasisi zilizo chini ya Ofisi yake, yenye lengo la kufahamu utekelezaji wa majukumu yao, kuimarisha mahusiano ya kikazi, pamoja na kutoa maelekezo ya kuongeza ufanisi, uwajibikaji na tija katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Aidha, Mhe. Sangu ameihimiza CMA kuendelea kukuza matumizi ya teknolojia katika kutatua migogoro ya kazi, ikiwemo kuboresha mfumo wa e-Utatuzi. Amesisitiza kuweka mazingira rafiki kwa watumiaji wa mfumo huo ili uwe nyenzo madhubuti ya kumaliza migogoro kwa wakati na kwa ufanisi.

Awali Naibu Waziri wa Ofisi hiyo, Mhe. Rahma Kisuo, ameitaka Tume kuendelea kujitangaza na kutoa elimu kwa umma kuhusu huduma zinazotolewa, pamoja na kuimarisha usawa na haki mahali pa kazi.

Kadhalika, amewataka watumishi wa Tume kuongeza jitihada katika kufanya usuluhishi kama njia ya msingi ya kutatua migogoro ya kikazi, akisisitiza kuwa mazungumzo yanarahisisha utoaji wa haki na kupunguza migogoro kazini.

Naye Mkurugenzi wa CMA, Bw. Usekelege Mpulla, amesema kuwa Tume itaendelea kuboresha matumizi ya teknolojia ili kuongeza ufanisi katika utatuzi wa migogoro ya kazi.